The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesMount Sinai [At-tur] - Swahili translation - Ali Muhsen Alberwany
Surah Mount Sinai [At-tur] Ayah 49 Location Maccah Number 52
Naapa kwa mlima wa T'ur!
Na Kitabu kilicho andikwa .
Katika ngozi iliyo kunjuliwa!
Na kwa Nyumba iliyo jengwa!
Na kwa dari iliyo nyanyuliwa!
Na kwa bahari iliyo jazwa!
Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.
Hapana wa kuizuia.
Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso!
Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,
Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu,
(Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!
Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu?
Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda.
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema,
Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni.
Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda.
Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini.
Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma.
Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda.
Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi.
Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza.
Wataelekeana wakiulizana.
Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa;
Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto.
Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.
Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu.
Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari.
Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.
Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu?
Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini!
Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli.
Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?
Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini.
Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka?
Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi!
Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana?
Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama?
Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika?
Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka.
Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye.
Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana.
Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa.
Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa.
Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui.
Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama,
Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota.