The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe moon [Al-Qamar] - Swahili translation - Ali Muhsen Alberwany
Surah The moon [Al-Qamar] Ayah 55 Location Maccah Number 54
Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!
Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea.
Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti.
Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio.
Hikima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu!
Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha; .
Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika!
Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu.
Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa.
Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!
Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika.
Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa.
Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba.
Ikawa inakwenda kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa.
Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka?
Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu.
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka?
Kina A'di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo,
Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng'olewa.
Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye kumbuka?
Thamudi waliwakanusha Waonyaji.
Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!
Ni yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi!
Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi.
Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili.
Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika.
Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.
Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!
Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa.
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye?
Kaumu Lut'i nao waliwakadhibisha Waonyaji.
Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut'i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri.
Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru.
Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo.
Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu!
Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea.
Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!<
Na hakika tumeisahilisha Qur'ani kuikumbuka. Lakini yupo anaye kumbuka?
Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni.
Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza.
Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani?
Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu.
Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma.
Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi.
Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu.
Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu!
Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.
Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.
Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anaye kumbuka?
Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni.
Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito.
Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza.