The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe reality [Al-Haaqqa] - Swahili translation - Ali Muhsen Alberwany
Surah The reality [Al-Haaqqa] Ayah 52 Location Maccah Number 69
Tukio la haki.
Nini hilo Tukio la haki?
Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki?
Thamudi na A'di waliukadhibisha Msiba unao situsha.
Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno.
Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika.
Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani.
Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki?
Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia.
Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu.
Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina,
Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi.
. Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu,
Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja,
Siku hiyo ndio Tukio litatukia.
Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa.
Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi.
Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote yenu.
Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!
Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu.
Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza,
Katika Bustani ya juu,
Matunda yake yakaribu.
Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita.
Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu!
Wala nisingeli jua nini hisabu yangu.
Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa.
Mali yangu hayakunifaa kitu.
Madaraka yangu yamenipotea.
(Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu!
Kisha mtupeni Motoni!
Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini!
Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu,
Wala hahimizi kulisha masikini.
Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu,
Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni.
Chakula hicho hawakili ila wakosefu.
Basi naapa kwa mnavyo viona,
Na msivyo viona,
Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima.
Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini.
Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka.
Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu,
Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia,
Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo!
Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia.
Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu.
Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha.
Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa.
Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini.
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu.